Art for Peace Submissions

Art for Peace Submissions

SHAIRI by MULMAT HAMAD RAJAB

Published

May 16, 2026

Author

Sylvia Moraa

Organization

IPPNW

TIBA YA NAFSI

Sitini sasa nagonga, ya maisha niloishi
Huzuni imeninyonga, kwa fikira za mazishi
Ni juzi tu nimejenga, sijavinjari aushi
Ndo sasa ninajipanga, mali yangu kuidishi.
Sababu ya kuchelewa, ya mlalahai kuwa
Kwa muda nimeugua, maradhi yalonitua
Si mahoma ya mafua, ama kibovu kifua
Ni kutwa kujiumbua, maumbile nilopawa.
Na hilo lilichochewa, na kule kujicompare
Warembo walomezewa, kwa simu 'kiangalia
Tete hali ikakuwa, waja wakiniambia
Siwezi kutamaniwa, hivyo nikajichukia.
Nikajiona kinyaa, njiani nikitembea
Nikaona ninafaa, mate wakinitemea
Nikawa nawaduwaa, walionikurubia
Na kuwaona shujaa, wema wakinitendea.
Mapenzi 'liyakataa, hata nilipopatiwa
Kwa hofu tu kunijaa, wanafiki watakuwa
Peke yangu nikakaa, 'kidhani 'takuwa sawa
Ila ikawa balaa, mvivu nilipokuwa.
Ajizi nyumba ya njaa, walidokeza wahenga
Kwa ukame kunivaa, nikawa sasa nafunga
Nikazidi kusinyaa, maradhi yakanilenga
Roho yangu ikapaa, nikifa hali mchanga.
Ndo hapo kajiketisha, 'kutafuta langu kosa
La mtu 'kiwa atisha, anapaswa kujitesa
Amani kajikosesha, kwa mawazo yangu tasa
Ya umbile kuridhisha, ni bora kuliko pesa
Kuanza kujikubali, 'livyoumbwa na Jalali
Ilikuwa si sahali, mi kufanya jambo hili
Ila 'kapata morali, ilipoboreka hali
Nikanawiri kimwili, pamoja na kiakili.
 

Malenga: Mulhat Hamad