Kwenye kambi ya wakimbizi, mpakani pa nchi, kunatokea kijana mmoja anayesimulia athari ya vita vilivyotokea kwao, na vilivyowasababisha kuwa wakimbizi wa nchi yao. Anasimulia madhila wanayopitia kwenye kambi. Kambi ile inajumuisha vijana, wazee, ajuza hasa, Watoto wachanga na wengine wengi. Japo mapito yale ni ya kutamausha, miale ya matumaini inaonekana ikiwakodolea macho, pengine ‘siku njema’ ikawadia.
KAMBI YA WAKIMBIZI
Ninakumbuka vyema,
Siku ile ya ‘kiama’,
Mabomu yakirushwa,
Risasi zikifyatuliwa,
Majengo yaliporomoshwa,
Vijiji vikisambaratishwa,
Kote kukilipuka,
Mioto kutawala.
Tulijaribu kuhepa,
Ila Izraili alijikaza,
Bado nakumbuka,
Wazazi wangu wakichomeka,
Wanuna wangu bila shaka,
Risasi zikiwapata,
Taswira ile i hai,
Kijiji kikiangamia.
Muda ukipita,
Wakatili wakafika,
Kwa visu na mapanga,
Kazi yao kukamilisha,
Haya sikushuhudia,
Rafiki amenieleza,
Sijui nilipokuwa,
Pengine kaniokoa Malaika.
Kutoka vijiji vyetu vizuri,
Hadi kambi ya wakimbizi,
Kutoka majumba yetu ya kifahari,
Hadi mahema ya karatasi,
Sauti ya vicheko na amani,
Sasa vilio vimebakia,
Shida jua linapochomoza,
Taabu giza likitanda.
Ajuza yule jamani,
Anavyolemewa na baridi,
Blanketi lake jepesi,
Kumsaidia haliwezi,
Mkongojo wake kwake rafiki,
Jamaa zake wakiwa vumbi,
Akipoteza tumaini,
Kuchukua za mwisho pumzi.
Kijana yule tazama,
Alivyoshika tama,
Mguu mmoja hana,
Wakatili walimnyang’anya,
Namtazama kwa huruma,
Japo siwezi kumsaidia,
Chozi lamdondoka,
Hawezi kufarijika.
Vitoto hivyo vyalia,
Kama mimi ni yatima,
Nani atavinyonyesha?
Vingali vichanga,
Itakuaje hii dunia?
Bila sauti ya mama,
Ilishachaguliwa yao hatima,
Na migogoro ya watu wazima.
Watoto wanalia,
Wazee wakikohoa,
Vibanda vimebanana,
Hamna nafasi ya kupumua,
Ardhi ngumu yetu kitanda,
Twaumia japo twavumilia,
Japo yabana kifua,
Maisha yanaendelea.
Jua linapotokea,
Tumbo lalilia haki,
Haki itoke wapi?
Pengine mara moja kwa wiki,
Tumekonda na kukondana,
Nguvu zimetuishia,
Tumbo linanguruma,
Itabidi livumilie.
Siku njema,
Yamewasili malori ya misaada,
Yanazo nafaka,
Umati ukikusanyika kupokea,
Nyusoni tuna furaha,
Miale ya matumaini,
Muda si muda,
Tukianza kung’ang’ania.
Wenye nguvu wananyakua,
Wazee wanalemewa,
Mchezo huo ukiendelea,
Tunazidi kujeruhiwa,
Hawa utu hawana,
Vyote wakitaka,
Kwa utulivu tunawasihi,
Angalau kila mtu apate.
Kwenye magumu haya,
Pengine tumaini lipo,
Pengine tukarudi vijijini,
Tukazika ‘vumbi’,
Kwani hakukuwa nafasi,
Hata ya kuomboleza,
Wakiingia mazungumzoni,
Ndoto hii kutimiza.
Itakuwa siku njema,
Amani itakaporejea,
Tukiondoka kambini,
Kuondokea hili jinamizi,
Liwafikie ofisini,
Walilosababisha hili,
Mola anawaona,
Uovu waliotutenda.
Itakuwa siku njema,
Majirani kusalimiana,
Mioyo ikipona,
Maisha yanaendelea,
Ya kale tukisahau,
Usoni tukiganga,
Lisitufikie tena,
Libaki tu historia.
Onyando Emanuel Ochieng’
C3/1482/2024
emanuelonyando@students.uonbi.ac.ke
0706760212
